Hii ni mara ya
pili kwa Dk Slaa kuzungumza na gazeti hili, lakini akikatakaa kufafanua
mambo mbalimbali yanayohusu sakata lake na Chadema, akiahidi kuwa
kufanya hivyo baadaye, huku akiweka bayana kuwa hajawahi kuwa na akaunti
ya twitter.
Dk Slaa, aliyekuwa anatajwa kuwa mgombea
urais wa Chadema, hajaonekana hadharani katika matukio makubwa ya
kichama tangu Chadema na Ukawa walipomkaribisha waziri mkuu wa zamani,
Edward Lowassa na kumteua kuwa mgombea urais anayeungwa mkono na vyama
vinne vinavyounda umoja huo.
Mara ya mwisho kuonekana kwenye shughuli za chama hicho ni
katika kikao cha Kamati Kuu wakati Lowassa alikaribishwa kufanya
majadiliano na kujibu hoja za wajumbe.
Lakini baada ya
hapo Dk Slaa hakuonekana wakati wa kutambulishwa kwa Lowassa kwa
waandishi wa habari, tukio la kuchukua na kurudisha fomu za urais ndani
ya chama na tukio la juzi la kuchukua fomu za urais kutoka Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC).
Wakati hayo yakiendelea, kuna
akaunti ya twitter yenye jina la “Dr Willibrord Slaa” ambayo imekuwa
ikitoa kauli mfululizo zikiwa na ujumbe mbalimbali unaoendana na
mazingira aliyomo sasa mwanasiasa huyo.
Agosti 10, kulitumwa ujumbe zaidi mara 10, mmojawapo ukijaribu kuwaaminisha watu kuwa hiyo ni akaunti halisi ya Dk Slaa.
“Ndugu
zangu Watanzania, hii ni akaunti yangu rasmi, bila shaka yoyote na
naomba ninachoandika hapa kifikishwe kwa Watanzania popote walipo,”
unasema ujumbe huo.
Taarifa nyingine zilizotumwa kwenye
akaunti hiyo ya twitter ni pamoja na ile iliyoeleza kuwa Dk Slaa
ameomba ulinzi kutoka nchi na mashirika ya kimataifa na atazungumza
kupitia runinga na redio pindi atakapopata ulinzi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Slaa alisema hajawahi kutuma taarifa yoyote kwenye mitandao ya kijamii.
“Sijawahi ku-operate (kuendesha) kitu chochote kwenye akaunti ya twitter, sina akaunti kama hiyo,” alisema Dk Slaa.
Mbali
na kukanusha kumiliki na kuendesha akaunti hiyo, Dk Slaa alirudia kauli
yake ya wiki iliyopita kuwa atatoa msimamo wake muda muafaka
utakapofika, baada ya kuulizwa swali kuhusu hatma yake ndani ya Chadema
na kisiasa kwa ujumla.
“Subira yavuta heri, sasa ili
uipate hiyo heri unatakiwa kuvumilia. Kwa hiyo wakati ukifika
nitazungumza tu na Watanzania,” alisema.
Alipoulizwa ni
wapi alipo kwa sasa, alisema yupo Dar es Salaam anapumzika, lakini
akasisitiza kuwa ipo siku ataweka wazi mustakabali wake kisiasa.
Dk
Slaa alisema yeye na mke wake Josephine Mushumbusi wanatarajia kusafiri
kwenda nje ya nchi katika siku chache zijazo, ingawa hakuweka wazi nchi
anayotarajia kuitembelea, lakini akasema atarejea baada ya wiki moja.
Post a Comment